Alhamisi , 7th Feb , 2019

Hatimaye bodi ya ligi (TPLB) imeweka wazi kuwa moja ya tatizo kubwa linaliosababisha kubadilishwa kwa ratiba ya ligi kuu ni timu kutokuwa na viwanja vyake ambapo katika timu 20 za ligi kuu zinazomiliki viwanja ni tano pekee na Yanga na Simba si miongoni mwao.

Wachezaji wa Yanga na Simba

Akiongea kwenye mahojiano maalum na www.eatv.tv, Mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi Boniface Wambura amesema tangu kuanza kwa msimu wa 2018/19 ni viwanja vitano pekee ambavyo havijabadilishiwa mechi.

''Suala la ligi kubadilika lipo tu na sio kwa matakwa yetu muda mwingine ni changamoto ya matumizi ya viwanja ambapo mnaweza kupanga vizuri ratiba lakini uwanja ukabadilishiwa matumizi na kwakuwa klabu haikumiliki lazima ikubali kupisha'', amesema.

Aidha Wambura amezitaja timu 5 zinazomiliki viwanja kuwa ni Azam FC (Azam Complex), Mtibwa Sugar (Manungu), Mwadui FC (Mwadui Complex), Ruvu Shooting (Mabatini) na  JKT Tanzania (JKT Mbweni).

Wambura amesema kama timu zitamiliki viwanja vyake itapunguza ratiba kubadilika mara kwa mara tofauti na sasa ambapo mechi moja tu ikibadilika inakuwa na athari za moja kwa moja kwenye michezo mingine.